TAARIFA KWA UMMA
A: TATHMINI NA MWELEKEO WA MIFUMO YA HALI YA HEWA
JANUARI HADI MACHI 2013.
Katika kipindi cha mwezi Januari hadi Machi 2013, hali ya joto la bahari katika ukanda wa tropikali ya mashariki na magharibi mwa bahari ya Pasifiki inatarajiwa kuwa ya wastani hadi chini ya wastani. Hali kadhalika, joto la bahari katikati ya bahari ya Hindi linatarajiwa kuwa chini ya wastani wakati joto la bahari karibu na pwani ya Tanzania linatarajiwa kuwa la wastani hadi juu ya wastani. Hali hii inatarajiwa kusababisha upepo wenye unyevunyevu kuvuma kutoka bahari ya Hindi kuelekea katika maeneo ya ukanda wa Pwani. Vilevile, joto la bahari katika bahari ya Atlantiki, kusini magharibi mwa bara la Afrika linatarajiwa kuwa la chini ya wastani na hivyo kusababisha upepo kutoka magharibi kuvuma kuelekea maeneo ya kusini magharibi mwa nchi.
B: MWELEKEO WA MVUA KWA MWEZI JANUARI HADI MACHI 2013
Mvua kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Machi, 2013 zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani, isipokuwa maeneo ya kaskazini magharibi ambayo yanatarajiwa kuwa na mvua za wastani hadi chini ya wastani. Aidha mchanganuo wake ni kama ifuatavyo;
Maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua (Pwani ya Kaskazini, Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki ukanda wa ziwa Victoria):
Baadhi ya maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka (Mikoa ya Dar es salaam, Tangam Pwani, Arusha, Kilimnjaro, Manyara, Mwanza, Mara, Geita, Shinyanaga, Kagera na Simiyu) yanatarajiwa kupata mwendelezo wa mvua (out of season rains) mwezi Januari. Aidha utabiri wa mvua za masika katika maeneo haya utatolewa mwezi Februari, 2013.
Mvua za Msimu
Kipindi cha mvua za Msimu Novemba hadi Aprili ni mahsusi kwa maeneo yanayopata mvua mara moja kwa mwaka (Kanda ya Magharibi, Kanda ya kati, Nyanda za juu kusini magharibi, mikoa ya kusini na pwani ya kusini). Mvua zinaendelea kunyesha na kwa kipindi cha Januari hadi Machi, 2013 zinatarajiwa kuwa kama ifuatavyo;
Kanda ya Magharibi (Mikoa ya Tabora, Katavi na Kigoma):
Mvua zinatarajiwa kuwa za wastani.
Kanda ya kati (Mikoa ya Singida na Dodoma):
Mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani.
Nyanda za juu Kusini Magharibi: (Mbeya, Rukwa, Iringa na Morogoro-kusini ):
Mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani.
Kanda ya kusini na Pwani ya kusini (Mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi):
Mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu wastani.
MUHIMU: Aidha katika maeneo mengi ya nchi kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa viwango vya mvua ya wastani vinaendelea kushuka, hivyo kufanya mvua za wastani katika baadhi ya maeneo kutokidhi mahitaji ya shughuli mbali mbali kama vile kilimo, maji na nishati.
Taarifa inaonyesha kwa mfano maeneo ya kusini uwezekano wa kupata mvua za juu ya wastani ni asilimia arobaini 40%, mvua za wastani 35% na mvua za chini ya wastani 25%.
D: ATHARI NA USHAURI
Kipindi cha mvua kilichobaki ni kifupi hivyo pamoja na matarajio ya mvua za wastani hadi juu ya wastani katika baadhi ya maeneo ya kati na kusini mwa nchi tunashauri maji yatumike kwa uangalifu hasa shughuli za umwagiliaji katika maeneo ya mito inayotiririsha maji kwenye mabwawa ya kuzalisha umeme ili kuwa na uhakika wa kupata maji ya kutosha katika mabwawa. Aidha vyanzo vya mito hiyo (cathment areas) vihifadhiwe na kuhakikisha hakuna uharibifu wa mazingira.
Kuna uwezekano wa kuwa na vipindi vifupi vya mvua kubwa zinazoambatana na upepo mkali katika kipindi hiki cha mvua hivyo tahadhari ziendelee kuchukuliwa ili kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao.Tunashauri pia wafugaji wajenge tabia ya kuhifadhi malisho kwaajili ya kutumia wakati kunapokuwa na upungufu wa malisho.
Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania Itaendelea kufuatilia Mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa pamoja na vimbunga katika bahari ya Hindi na kutoa taarifa kuhusiana na mwelekeo wa mvua nchini.
Imetolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania
No comments:
Post a Comment