Ndugu Wananchi,
Mtakumbuka kuwa hapo tarehe 23 Februari 2012
tuliwatangazia kupitia vyombo vya habari juu ya usitishwaji wa matangazo ya
televisheni kwa kutumia teknolojia ya analojia kwenda katika mfumo mpya
unaotumia teknolojia ya dijitali.
Napenda kuwaleleza kuwa, maandalizi ya kuzima
mitambo ya analojia kuanzia tarehe 31 Desemba 2012 yamekamilika kwa mujibu wa
makubaliano ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Hata hivyo, napenda sasa kutoa taarifa kuwa
uzimaji wa mitambo ya analojia utafanyika kwa awamu kama ifuatavyo:-
(1) Dar Es Salaam-31 Desemba, 2012;
(2) Dodoma & Tanga- 31 Januari, 2013;
(3) Mwanza-28 Februari, 2013;
(4) Moshi & Arusha-31 Machi, 2013;
(5) Mbeya-30 Aprili, 2013.
Tumeamua kuanza kuzima mitambo hiyo kwa Jiji la
Dar es Salaam kwanza ili kutoa fursa kwa makampuni yenye leseni kusimika
mitambo ya utangazaji wa dijitali katika mikoa mingine. Makampuni haya
yamejipanga kukamilisha usimikaji wa mitambo hiyo katika mikoa minane katika
miezi minane ijayo.
Mitambo ya analojia itakayozimwa kesho ni ile
iliyopo Kisarawe na Makongo. Vituo ambavyo siku ya tarehe 1 Januari 2013,
vitapaswa kuanza kutangaza matangazo kwa mfumo wa dijitali ni TBC1, ITV, EATV,
Channel 10, StarTV, DTV, CapitalTV, TumainiTV, ATN, MlimaniTV, C2C, CTN,
CloudsTV na Efatha.
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inafanya
jitihada za kutosha kuhakikisha kwamba makampuni yenye leseni za kusambaza
ving’amuzi yanakuwa na ving’amuzi vya kutosha na vingine vimeagizwa ili kukidhi
mahitaji ya baadaye na vile vilivyopo sokoni vina ubora unaokubalika.
Vilevile, Serikali kwa kushirikiana na Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania itahakikisha kwamba zoezi la uhamaji linafanyika bila
usumbufu na kero kwa wananchi. Makampuni yanayouza ving’amuzi yameagizwa
yaimarishe huduma kwa wateja wakati wa kuuza ving’amuzi na hata baada ya
ununuzi iwapo wananchi watakuwa na matatizo na ving’amuzi.
Zoezi hili la uhamaji ni muhimu sana kwa maendeleo
ya nchi yetu. Tutakapokuwa tumekamilisha uhamaji, huduma za mawasiliano na
utangazaji zitapanuka na kuwa bora zaidi. Kwa mfano, itawezekana sasa kuangalia
televisheni kupitia simu zetu za mikononi. Vilevile, itawezekana, kwa bei nafuu
kabisa, kwa mtu mwenye uwezo wa kutengeneza vipindi kukodisha chaneli yake na
kutangaza vipindi vyake. Vilevile, bei za mawasiliano na utangazaji zitashuka,
na tutakuwa tumepiga hatua kubwa kwenye mapinduzi ya teknolojia duniani, ambayo
nchi yetu haiwezi kubaki nyuma.
Ndugu Wananchi,
Serikali kwa kushirikiana na Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania itaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu uhamaji huu.
Serikali inatarajia kupata ushirikiano wa karibu kutoka kwa wadau wa sekta ya
utangazaji na wananchi kwa ujumla katika kipindi cha uzimaji wa mitambo ya
utangazaji wa televisheni ili kufanikisha zoezi la uzimaji wa mitambo ya
utangazaji ya teknolojia ya analojia.
Uhamaji huu hautahusu televisheni za wananchi
zinazopata matangazo kupitia madishi (nyungo) (satellite) au nyaya (cables).
Hivyo, wananchi wanaopata matangazo kupitia DStv, Zuku, na nyinginezo
wataendelea kupata matangazo yao kama kawaida.
Ndugu Wananchi
Kama kuna mwananchi yoyote ana kero, malalamiko,
swali au anahitaji maelekezo kuhusu uhamaji, awasiliane na Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania (TCRA) kupitia namba 0784-558270; 0784558271 au barua
pepe: malalamiko@tcra.go.tz
No comments:
Post a Comment